Na Moshi said, 26 Agosti 2024
Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira imepanga kufanya Mkutano na viongozi, wataalamu na wadau wa Mazingira na mabadiliko ya tabianchi Septemba 09 hadi 10 , 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Jijini Dodoma,ikiwa lengo ni kujadili changamoto za Mazingira.
Taarifa hiyo imetolewa leo Agost 26,2024 Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt Ashantu Kijaji wakati akizungumza na Waandishi wa habari,nakusisitiza kuwa kumekuepo na changamoto mbalimbali za Mazingira ambazo zinafifisha ustawi wa jamii na uchumi, ikiwa ni pamoja uharibifu wa ardhi, vyanzo ya maji, ukataji miti ovyo na uharibifu wa misitu.
Dkt.Kijaji amesema kuwa Mazingira na Maliasili ni msingi wa uhai wa binadamu , hivyo usimamizi na hifadhi ya rasilimali hizo ni suala la kipaumbele na lenye umuhimu wa kipekee.
Aidha, amesema kuwa changamoto za uharibifu wa Mazingira unasababisha upotevu wa makazi ya wanyamapori na bayoanuai; athari za mabadiliko ya tabianchi; uharibifu wa mifumo-ikolojia ya pwani na baharini; uharibifu wa ardhi oevu; uchafuzi wa mazingira; na kuenea kwa viumbe vamizi.
"Changamoto hizi zinachangiwa na shughuli za binadamu zisizo endelevu ikiwemo utegemezi mkubwa wa kuni na mkaa kama chanzo cha nishati; kilimo kisicho endelevu; utupaji taka ovyo; na ufugaji wa mifugo usiowiana na maeneo ya malisho"amesema.
Nakuongeza kuwa "Changamoto nilizozitaja hapo awali zinaathiri sekta muhimu za uchumi kama vile kilimo, nishati, maji, uvuvi na utalii; ustawi wa jamii na viumbe hai, hivyo, kwa kutambua mchango wa wadau katika kuhifadhi na kusimamia mazingira na mabadiliko ya tabianchi nchini"
Amesema kuwa Mkutano huo unalenga kuimarisha uwajibikaji, ufanisi na usimamizi wa hifadhi ya mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Ameendelea kufafanua kuwa Mkutano huo unatarajia kushirikisha wadau zaidi ya 1,000 kutoka katika Wizara na Taasisi za Serikali; Mashirika ya Umma, Sekta binafsi, vyuo vya elimu ya juu na Asasi zisizo za Serikali.
"Viongozi watakaoshiriki Mkutano huu ni Mawaziri na Makatibu Wakuu kutoka Wizara za Kisekta; Wakuu wa Mikoa; Wakuu wa Wilaya; na Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Tanzania Bara. Vile vile, Mkutano utashirikisha Wakurugenzi kutoka katika mashirika ya Umma na wataalamu; Sekta Binafsi; na Asasi zisizo za kiserikali."
Aidha amesema kuwa Mkutano huo utajadili fursa zilizopo katika hifadhi na usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Hii ni pamoja na Biashara ya Kaboni; usimamizi wa taka; mabadiliko ya tabianchi; nishati safi ya kupikia; upandaji miti na usimamizi na uzingatiaji wa Sheria nchini.
Waziri Kijaji ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa jitihada anazofanya kuimarisha hifadhi na usimamizi wa mazingira nchini.
"Mheshimiwa Rais ameendelea kusimamia na kutoa mwongozo mahsusi katika kuhakikisha kuwa Mazingira na Maliasili zinahifadhiwa na kuongeza mchango katika pato la Taifa.
Comments
Post a Comment