Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya ya Wilaya ya Busega ambae pia alikuwa Msimamizi wa Uchaguzi Mkuu Jimbo la Busega, Bw. Anderson Njiginya Kabuko leo tarehe 17/11/2020 amekutana na wawakilishi wa Vyama vya Siasa vilivyoshiriki Uchaguzi Mkuu uliofanyika mapema mwezi Oktoba mwaka huu.
Kikao hicho kimefanyika Shule ya Msingi Nyashimo, ambapo wawakilishi wa Vyama vya Siasa waliomba kukutana na Msimamizi wa Uchaguzi, huku wakidai kwamba sababu ya kufanya hivyo ni kuendeleza ushirikiano wao kwa pamoja.
“Tulianza pamoja, hivyo ni vyema kukaa pamoja baada ya Uchaguzi kumalizika ili kuzungumza masuala ya kimsingi kama tulivyoanza na tulivyokuwa pamoja kipindi chote cha Uchaguzi”, mmoja wa wawakilishi aliongeza.
Katika kikao hicho kilichokuwa cha takribani muda wa saa moja kimeshuhudia wawakilishi wa Vyama vya Siasa wakimshukuru Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Busega na timu yake yote walivyosimamia Uchaguzi kwa uhuru na uwazi na kuahidi kuendelea kushirikiana nae kwaajili ya maendeleo ya Wananchi wa Busega.
Pia wamekiri kwamba hali ya upendo na mshikamano wao kama Vyama vya Siasa inatokana na kujali maslahi ya Wananchi wa Busega na sio vinginevyo. Aidha, wamepongeza vyombo vya Ulinzi Wilayani Busega kwa kusimamia amani kwa kipindi chote cha Uchaguzi.
Awali, Kabuko amevishukuru Vyama vya Siasa kwa kuonesha utulivu katika kipindi chote cha Uchaguzi na hata baada ya Uchaguzi kumalizika. “Uchaguzi umekwisha, tuweke tofauti zetu pembeni sasa tuwahudumie wananchi wa Busega”, aliongeza Kabuko.
Kwa upande mwingine wawakilishi hao wa Vyama Siasa wameomba kushirikishwa katika masuala ya Maendeleo kwani wao wapo tayari kushiriki na kusisitiza kwamba wao ni wadau wakubwa wa Maendeleo.
Wawakilishi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), ACT Wazalendo, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Civic United Front (CUF) walihuhudhiria kikao hicho. Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi Mkuu ngazi ya Jimbo na Afisa Uchaguzi wa Wilaya ya Busega.
Comments
Post a Comment