Afisa wa TGNP Mtandao Jackson Malangalila akitoa ufafanuzi wa jambo fulani katika semina ya kuwajengea uwezo wananchi kupinga ukatili wa kijinisia.
Ukatili wa kijinsia hasa kwa watoto umeendelea kuwa changamoto kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Hayo yamebainishwa na baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es salaam waliposhiriki katika Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) zinazofanyika kila wiki katika ofisi za TGNP Mtandao.
Akiongoza semina hiyo Afisa wa shirika hilo Bw. Jackson Malangalila amesema ili kuweza kukabiliana na changamoto za ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto ni vema wanajamii kuweza kuwa na nguvu ya pamoja katika kukabiliana tatizo hilo.
Malangalila ameendelea kusisitiza kuwa mkiwa na nguvu za pamoja ni rahisi hata kuweza kudai jambo Fulani katika Serikali ya mtaa, Polisi hata Mahakamani na mkaweza kushinda kutokana na umoja wenu, lakini kila mtu akifuatilia kesi mwenyewe ni ngumu kupata ushirikiano wa kutosha mahala husika.
Semina ikiendelea.
Ameongeza kuwa changamoto kubwa ya wanaharakati wamekuwa wakifanya mambo wenyewe wenyewe hali inayoweza kuwaletea matatizo hapo baadae, kwani wanaweza kuundiwa hata tuhuma za kuonekana wanataka kuchafua chombo husika ama kuleta machafuko.
Kwa upande wake Mwanaharakati Zahara Omary kutoka Kivule amesema kuwa changamoto kubwa kwenye harakati ambayo inawafanya wengi kushindwa, ni kwamba kwenye harakati unatumia muda mwingi na fedha nyingi kama nauli katika kufuatilia kitu kimoja ambacho ukizingatia hakina maslahi mapana kwako na kwa familia yako.
Ameongeza kuwa unaweza ukamsaidia mtu ambaye huna hata undugu wala ujamaa nae, na kesi ikifika polisi unaambiwa uje umalizane na mtuhumiwa na muda mwingine unatangaziwa pesa nyingi kiasi ambacho ukiwa na roho nyepesi unachukua na kuachana na ufuatlialiaji wa kesi hiyo.
Baadhi ya washiriki wengine wameendelea kulalamikia tatizo la wazazi kumalizana na watuhumiwa hivyo kumpunguza nguvu mfuatiliaji wa kesi hiyo hali inayomfanya mwanaharakati kuonekana kama anaingilia mambo yasiyomuhusu.
Na changamoto nyingine kubwa imeonekana ni baadhi ya watekelezaji wa ukatili ni watu wenye wakubwa na wenye mamlaka makubwa serikalini hivyo kusababisha ugumu katika kuendesha kesi kwani mala nyingine utishia hata kuwapoteza wanaolivalia njuga suala hilo.
Comments
Post a Comment