Na Isack Magessa, DSM
Shirika la reli Tanzania (TRC) limesaini mkataba wa ununuzi wa mashine na mitambo ya matengenezo ya njia ya reli ya kisasa SGR, ambapo mashine hizo zitakuwa 26 zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 51.
Akiongea kwa niaba ya Shirika hilo leo Novemba 7 - 2022, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa amesema kuwa TRC imeingia mkataba wa ununuzi wa mashine na mitambo hiyo ya matengenezo ya njia ya reli ya SGR na kampuni na Kampuni ya Sung Shin Rolling Stock Technology (SSRST) ya Korea Kusini.
Aidha amesema mkataba huo ni Sehemu moja wapo ya kuelekea katika mchakato wa kuanza rasmi kwa uendeshaji wa kutoa huduma za usafirishaji wa treni ya SGR mpaka kufikia mwezi Aprili 2023.
Amesema kuwa lengo la ununuzi wa mashine na mitambo hiyo ni kuongeza ufanisi wa matengenezo ya njia na kupunguza kufanya matengenezo ya njia kwa kutumia watu ambapo mitambo hiyo italipa uwezo shirika katika kutunza reli hiyo ya kisasa ya SGR.
Hata hivyo ameongeza kuwa utekelezaji wa mkataba huo ambao utahusisha utengenezaji,mafunzo, makubaliano na makabidhiano unatarajiwa kufanyika kwa miezi 12.
Kuhusu nauli za treni hiyo ya kisasa itakayotumia umeme katika uendeshaji wake,Bw Masanja amewaondoa hofu watanzania kwa kusema kuwa nauli hizo zitaendana na mahitaji ya watanzania na zitakuwa nafuu kwao ambapo kwa sasa watazunguka katika mikoa mbalimbali kuzungumza na wananchi pamoja na wadau mbalimbali juu ya kupanga kiwango cha nauli hizo kutokana na watakavyokubaliana nao wakishirikiana na mamlaka ya usafiri wa ardhini Latra.
"Niwahakikishie watanzania kwa bei ambazo tutakuja nazo kila mtanzania ataweza kuzimudu na zitaendana na mahitaji ya watanzania na tumejipanga kwa hilo kuhakikisha tunatoa huduma bora na za kisasa katika mradi huu wa treni ya mwendokasi (SGR)"amesema Kadogosa.
Naye mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa shirika hilo John Kandoro amesema kuwa mitambo ambayo itanunuliwa na shirika hilo kupitia mkataba huo uliosainiwa hii leo utasaidia shirika hilo kuachana na matumizi ya kizamani ya njia za reli (washika vibendera)na kuja na matumizi ya kiteknolojia ambayo yatakuwa mwarobaini wa sekta ya usafirishaji kwa njia ya reli mchini na yatachangia TRC Kuendeshwa kisasa.
Aidha ameongeza kuwa mitambo hiyo itaendana na reli mpya ya kisasa na kuongeza kuwa kampuni ya (SSRST) itakuwa ikisaidia Sehemu ya marekebisho ya reli ya kisasa kupitia mitambo hiyo sambamba na kutoa mafunzo ya kutumia mitambo hiyo kwa wahandisi na mafundi wa kitanzania ili kuongeza ufanisi wa matumizi yake.
Hata hivyo amesema bado shirika litaendelea kutoa huduma za usafirishaji wa reli kupitia treni za reli ya kawaida ambazo zinaendelea kutoa huduma hivi sasa.
Mkataba wa makubaliano hayo baina ya shirika la reli Tanzania TRC na kampuni ya Sung Shin Rolling Stock Technology SSRST ya nchini Korea umesainiwa mbele ya viongozi mbalimbali wa Shirika hilo na makamo wa Rais wa kampuni ya SSRST,K.Charles PARK na balozi wa nchi ya Korea kusini hapa nchini,Balozi Kim Sun Pyo.
Comments
Post a Comment