Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam kufanya Mbio za Hisani za Pugu Marathon Mei 27

Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam limesema limeandaa Mbio za Hisani za Pugu Marathon zinazotarajiwa kufanyika Mei 27 mwaka huu.


Hayo yamebainishwa na Askofu Mkuu Jimbo Kuu la Dar es Salaam Jude Thadaeus Ruwa’ichi, O.F.M akizungumza na waandishi wa habari.

“Mbio hizi zitafanyika Siku ya Jumamosi ya tarehe 27 Mei 2023 kuanzia saa 12 asubuhi,” amesema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.

Askofu Mkuu Ruwa’ichi amesema lengo la kuu la mbio hizi ni kusaidia kupata majitoleo kwa ajili ya kuendeleza kituo chao cha hija kinachopatikana Pugu, kudumisha afya pamoja na kujenga utamaduni wa michezo.

Amebainisha kuwa mbio hizo zitakuwa za aina nne ambazo ni matembezi ya kilomita 2 ada ya ushiriki Sh 20,000, mbio fupi za kilomita 5 ada ya ushiriki Sh 20,000, mbio za kilomita 10 ada ya ushiriki Sh 30,000, na mbio za kilomita 21, ada ya ushiriki Sh 30,000.

“Ninawiwa kuwaomba wadau wa michezo hasa huu wa riadha, kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizi. Pia mashirika, makampuni, wafanyabiashara na washikadau wengine kujitokeza kutufadhili ili tuweze kufanikisha lengo kuu la mbilo hizi,” ameongeza Askofu Mkuu Ruwa’ichi

Comments