Naibu Waziri Mwakibete azindua Ripoti ya Sensa ya Vyombo Vidogo vya Usafiri wa Majini, aipongeza TASAC

Na Muandishi wetu 

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) Atupele Mwakibete amezindua Ripoti ya Sensa ya Vyombo Vidogo vya Usafiri Majini katika eneo la Tanzania Bara, 2021.

Akizungumza katika Hafla ya uzinduzi huo uliofanyika jijini humo, amelipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kufanikisha tukio hilo la kihistoria nchini.


“Ni jambo la kwanza katika historia ya Nchi yetu, ukanda wa Afrika Mashariki na Ukanda wa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kuhesabu vyombo Vidogo vya majini,” amesema Mwakibete.


Mwakibete amesema Kwamba vyombo Vidogo vya majini vina mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Hivyo ametumia fursa hiyo kuwataka Wadau mbalimbali hususan Serikali kutumia taarifa hiyo kuboresha Sera na mipango kuhusu vyombo vidogo vya majini na kuboresha katika matumizi ya usafiri wa majini.


Amewataka Wadau na TASAC kuitumia taarifa hiyo katika kushauri matumizi ya vyombo hivyo yanayoendana na maeneo husika ili kuepuka na kudhibiti ajali za majini.


Kadhalika Mwakibete ameitaka TASAC na wadau kuhakikisha wanatumia taarifa hiyo katika kuboresha utendaji wao.


“Niwaombe Wadau kutumia taarifa hizi za Sensa hii kuboresha utendaji katika Sekta ya uchumi hususan uchumi wa bluu,” ameongeza Mwakibete.


Mwakibete ameongeza kushauri kuwa Ripoti hiyo isaidia katika maboresho ya shughuli za uokoaji ajali zinapotokea majini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TASAC Kaimu Mkeyenge amesema kwamba Sensa hiyo uliofanyika kwa kutembelea maeneo ya mito, maziwa, Bahari na mabwawa kwa Tanzania Bara.


Kwamba maandalizi ya Sensa hiyo yalihusisha wataalam kutoka TASAC, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Wizara ya Uvuvi na Wizara Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).


Hivyo amesema wameanzisha kanzidata ya vyombo hivyo na taarifa zake kwa kubainisha wamiliki, mahali vilipo, matumizi yake, nyezo zake za mawasiliano, nyenzo zake za wokozi na kadhalika.


Kwa mujibu wa taarifa ya Ripoti hiyo ni kwamba idadi ya jumla ya vyombo vya majini nchini ni 52,189, idadi ya jumla ya mialo ya vyombo hivyo ni 885 na idadi ya vyombo hivyo vyenye urefu wa mita nne au zaidi ni 45,976.


Pia ripoti hiyo inabainisha kuwa asilimia 53% ya vyombo hivyo vipo Ziwa Victoria,  13.4% vipo Bahari ya Hindi, asilimia 10.2% Ziwa Tanganyika, 7.6% Ziwa Nyasa huku asilimia 1.5% vikipatikana maeneo mengine ikiwemo maziwa, mabwawa na mito.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Kaimu Abdul Mkeyenge amesema walishirikiana kuandaa ripoti hiyo na NBS, Wizara ya Uvuvi na Mifugo, Tawala za MIkoa na Serikali za Mitaa ambapo kwa pamoja walitoa wataalamu waliokwenda maeaneo husika kukusanya data.


Pia amesema sensa hiyo ilihitimishwa kwa kuandaa kazidata kwa kuangalia maeneo ya taarifa za vyombo, umiliki wa vyombo, matumizi ya vifaa, nyenzo za mawasiliano pamoja nyenzo zo uzimaji moto.


Nae, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo, Kapteni Mussa Mandia amesema sensa hiyo ni mara ya kwanza kufanyika nchini na kwamba vyombo vyote vilivyohesabiwa taarifa zake zimewekwa kwenye kanzidata.


Kapteni Mandia amefafanua kuwa ripoti hiyo itaumika katika kuimarisha usimamizi wa  usalama majini pamoja na kuchangia utungaji sera na mipango kwenye Uchumi wa Bluu.

Comments