Na Moshi Said
Waziri wa Maliasili na Utalii Angelah Kairuki amesema serikali itaendelea kuboresha maeneo mapya katika Makumbusho ya Taifa ikiwemo kuongeza jitihada katika suala la utafiti ili kuongeza tija na ufanisi katika sekta ya Utalii.
Waziri Kairuki amesema hayo Leo jijini Dar es salaam wakati alipofanya ziara ya kutembelea Makumbusho ya Taifa na Nyumba ya Utamaduni iliyopo Posta sambamba na Kijiji cha Makumbusho ili kuangalia utendaji kazi unaofanywa na kwenye Taasisi Hizo.
Aidha Waziri Kairuki amesema kuwa Makumbusho ya Taifa imesheheni utalii na utajiri mkubwa kwa taifa kutokana na kuhifadhi nyaraka muhimu ambazo zimekuwepo na zitaendelea kuepo kwa kizazi cha sasa na baadae.
‘Pia tunaendelea kuona ni kwa namna gani Malikale zetu tunaendelea kuziboresha na kuzikarabati lakini pia tuna Makumbusho takribani saba mpaka sasa na tumeanza kuwakaribisha watu binafsi ambao wapo tayari kuanzisha makumbusho zao binafsi yote ni kuendelea kutunza mila na tamaduni zetu na historia ili wageni waendelee kuvutika”amesema Waziri Kairuki
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga ameeleza mwongozo wa yeyote anayetaka kuanzisha makumbusho kuwa anapaswa kufata taratibu kwa kuandaa andiko linaloonyesha eneo husika.
Amesema maboresho ya sheria ya Mambo ya kale na Makumbusho ya Taifa yanaruhusu kuanzisha Makumbusho binafsi na hivyo wataalamu wanakwenda kuangalia eneo na kuandaa andiko na kuanza taratibu za kufanya usajili.
Naye Muhifadhi Historia Makumbusho ya Taifa kituo cha Nyumba ya Utamaduni Pius Gondeka amesema kuwa kazi yao wanayoifanya kama Makumbusho ni kuhifadhi hivyo ujio wa Waziri katika Makumbusho itaongeza chachu kwa Watanzania kutembelea taasisi hiyo.
Mhifadhi wa eneo linalohifadhi mifupa ya zamadamu (mwanadamu wa kale) Justin Nkungwe wamewahamasisha watanzania kuwa na desturi ya kutembelea makumbusho kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali.
Katika Ziara hiyo Waziri wa Maliasili na Utalii Angelah Kairuki ameambatana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Dunstan Kitandula ambapo imekuwa ni mwendelezo wa kutembelea taasisi mbalimbali zilizo ndani ya Wizara hiyo.
Comments
Post a Comment