Ujumbe wa Dkt. Kijaji kwa wawekezaji wazawa waliyopewa zabuni ya kuchimba Makaa ya Mawe Wilayani Ludewa

Na Moshi Said

Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt Ashatu Kijaji.

Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt Ashatu Kijaji amewataka wawekezaji Wazawa ambao wamepewa zabuni ya kuchimba Makaa ya Mawe katika mradi wa Mchuchuma Wilayani Ludewa Mkoani Njombe kufanya kazi kwa weledi mkubwa ili kufikia malengo ya Serikali ya uendelezaji wa miradi ya Kimkakati.

Waziri Dkt Ashatu amesema hayo Septemba 12,2023  Jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya utiaji saini wa Mikataba ya makubaliano kati ya Makampuni matano ya Wazawa na Shirika la Taifa la Maendeleo( NDC) ambayo yatatekeleza mradi wa Liganga na Mchuchuma kwakua ni maendelezo ya maono ya Serikali ya awamu ya sita ya kuendeleza sekta ya Viwanda na Biashara  hapa nchini.

 " Hii ni dhamira ya dhati naya hali ya juu ya serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha ndoto za utekelezaji wa mradi wa Liganga na Mchuchuma sasa zinatimia na rasilimali hizi ambazo zimekaa kwa muda mrefu bila kuwanufaisha wananchi ziwanufaishe na kuchangia katika uchumi wa nchi" amesema Dkt Ashatu

Aidha amesema kwamba Rais Dkt Samia Suluhu Hassan tayari ameridhia kutoa kiasi cha shilingi bilioni 15.4 ikiwa ni malipo ya fidia kwa wananchi wapatao 1142 ambao watapisha utekelezaji wa mradi huo ambao unatarajiwa kuanza kwa kufanyika utafiti  mapema mwezi huu.

 Wananchi 1142 wanatarajiwa kulipwa fidia,kati yao 1118 tayari wamelipwa fidia ,24 bado na kati yao 19 bado hawajulikani ,huku 5 wanakamilisha ili walipwe fidia zao,hivyo hawa 19 ambao hawajulikani mradi utakapoanza hawaonekani basi tutasitisha malipo yao" amesisitiza Waziri huyo wa Viwanda na Biashara Dkt Ashatu.

 Dkt Ashatu amesema kwamba kwa nyakati tofauti Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa akisema  ni wakati sasa umefika kwa rasilimali iliyopo katika miradi ya kimkakati ya Liganga na Mchuchuma kuanza uzalishaji na kwamba ni shauku yake kuona mradi huo wa muda mrefu unatekelezwa.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa shirika la Taifa la Maendeleo ( NDC) Dkt Nocolaus Shombe akiongea Septemba 12,2023  Jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya utiaji saini wa Mikataba ya makubaliano kati ya Makampuni matano ya Wazawa na Shirika la Taifa la Maendeleo( NDC)

Awali akizungumza  Mkurugenzi Mwendeshaji wa shirika la Taifa la Maendeleo ( NDC) Dkt Nocolaus Shombe amesema kuwa awali mchakato huo ulihusisha jumla ya Kampuni ishirini na tano (25) ambapo jumla ya kampuni kumi na saba( 17) zilifanikiwa kuwasilisha maombi yao kwa ajili ya uchambuzi na ushindani na hatimaye zilipatikana kampuni tano zilizokidhi vigezo.

 " Kampuni ishirini na tano ( 25) zilipewa nyaraka za zabuni kupitia mfumo wa ununuzi serikalini ( TANePS) ambapo kampuni 17 zilifanikiwa kuwasilisha nyaraka za zabuni,nakwamba kila kampuni itazalisha tani 30 kila mwezi sawa na tani 150 kwa kampuni zote tano kwa mwezi " amesema Mkurigenzi huyo Mwendeshaji wa NDC Dkt Shombe.

 Dkt Shombe ameendelea kusema kuwa mradi huo utakua na manufaa makubwa kiuchumi ikiwemo kutoa ajira zaidi ya mia tano za moja kwa moja ,ikirahisisha upatikanaji wa nishati inayotokana na makaa ya mawe kwa Viwanda hali ambayo itachochea ukuaji wa viwanda nchini pamoja na kuingiza fedha za kigeni kwa mkaa utakaouzwa nje ya nchi hususani nchi za jirani.

 Jumla ya kampuni tano zimetia saini makubaliano hayo ya uchimbaji wa makaa ya mawe katika mradi wa Mchuchuma ambazo ni Sheby Mix Investment Limited ,Nipo Engineering Company Limited,Chusa Mining Company Limited ,Kindaini Company Limited na Cleveland Mine and Service Company Limited ,mkataba ambao utadumu kwa muda wa miaka mitano.

Akizungumza kwa niaba ya Makampuni hayo Ndaisaba Ruhoro ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Cleveland Mine and Service Company Limited ameihakikishia serikali kuwa watafanya kazi kwa weledi mkubwa huku wakiipongeza serikali ya awamu ya Sita kwa kuweza kuwathamini na kuwaamini watanzania  katika kuwekeza kwenye miradi mbalimbali hapa nchini.

 " Kwa niaba ya wenzangu napenda kulishukuru shirika la Taifa la Maendeleleo ( NDC) Wizara ya Viwanda na Biashara na Serikali kwa ujumla kwa kutupa nafasi hii baada ya kukidhi vigezo mlivyoweka,tunamhakikishia Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa tutafanya kazi nzuri kwa weledi mkubwa kwa kuzingatia makubaliano ya kimkataba" amesema Ruhoro..

Comments