WAZIRI NDALICHAKO ATOA UJUMBE HUU KWA MAWAKALA BINAFSI WA AJIRA NDANI YA NJE YA NCHI

Na. Moshi Saidi, DSM

Serikali imewataka mawakala binafsi wa ajira ndani na nje  wanapowatafutia watanzania ajira nje ya nchi wazingatie utu  wasipofanya hivyo watachukuliwa hatua za kisheria pamoja na kuwafutia leseni zao

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na wenye ulemavu,Profesa Joyce Ndalichako.

Pia aliwataka mawakala hao kutovuka mipaka yao ya kazi ikiwemo kushikilia mishahara ya wafanyakazi waliowatafutia kazi huku wakichukua nusu ya mishahara hivyo  wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumza hayo jana Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na wenye ulemavu,Profesa Joyce Ndalichako alipokutana  na wakala binafsi wa huduma za ajira waliokuwa wakijadili namna ya kuongeza ufanisi na kutatua changamoto zinazowakabili,alisema 
mawakala hao wazingatie matakwa ya kisheria katika kuendesha shughuli zao.

Profesa Ndalichako alisema Serikali ilisitisha huduma za ajira nje ya nchi mwaka 2018 baada ya serikali kuona mawakala hao walikuwa wanaangalia kipato kuliko utu wa mtanzania.

Alisema mawakala hao wanapowapeleka watanzania nje ya nchi utu wa mtanzania uthaminiwe hivyo Serikali haipo tayari kuona wananyimwa stahiki zao,hawana mikataba na wakitaka kuondoka hawana uhuru wa kurudi nyumbani. 

"Nawasihi mawakala wote kuzingatia 
matakwa ya kisheria katika kuendesha shughuli zenu na wale wachache 
wanaokiuka misingi ya kisheria watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kumfutia leseni,"alisema Profesa Ndalichako.

Aidha alisema wako mawakala wachache wanaofanya shughuli hapa nchini ambao hawazingatii sheria ikiwemo kujihusisha na mahusiano ya kiajira na wafanyakazi wanaotakiwa kuwaunganisha na waajiri wanashindwa  kuwapatia wafanyakazi wao mikataba ya ajira na kutowachangia katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Profesa Ndalichako alisema  vitendo hivyo  ni ukiukwaji wa sheria za kazi pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Pia alisema Serikali Imeruhusu mawakala binafsi kuunganisha watanzania na fursa za ajira nje ya nchi kufanyika ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23 takribani mawakala 83 walisajiliwa kati ya hao 56  wamehuisha leseni zao kwa mwaka 2023/24.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Cyprian Luhemeja amewataka  mawakala hao kushirikiana na serikali kumaliza changamoto ya ajira nchi.

"Naamini leo tutajadiliana jinsi ya kuongeza ubunifu na ufanisi katika kuboresha na kumaliza  changamoto ya ajira nchini kwasababu Tanzania tumechelewa sana kupeleka watanzania nje ya nchi hivyo serikali inawaunga lakini kwa kufuata utaratibu mzuri wa kuwapeleka watanzania nje na utaratibu uwe wa leseni," alisema Luhemeja.

Mwakilishi wa mawakala binafsi wa Ajira ndani na nje ya nchi ,Bona Manyema alisema anaishukuru Serikali kwa kuwawekea mazingira wezeshi na wameahidi  kufuata tararibu hivyo atakayeenda tofauti na hayo atachukuliwa hatua za sheria.


Comments