Na Mwandishi wetu
MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inatumia maonesho ya 48 ya kimataifa ya kibiashara yanayoendelea Jijini Dar es Salaam kuhamasisha Umma wa watanzania wawekezaji na wageni kutoka mataifa mbalimbali kuwekeza katika maeneo inayoyasimamia huku ikijinasibu kuwa na fursa lukuki za uwekezaji
Akiongea na wageni waliotembelea banda la TAWA lililopo ndani ya banda la Wizara ya Maliasili na Utalii Afisa utalii Daud Tesha amesema TAWA ina uwanda mpana wa fursa za uwekezaji unaotoa mwanya kwa wawekezaji wa aina mbalimbali kuwekeza katika Taasisi hiyo
Akizitaja fursa hizo Tesha amesema yapo maeneo mengi yanayohitaji wawekezaji na uwekezaji katika Taasisi hiyo kama vile maeneo ya utalii wa picha kwenye maeneo ya hifadhi za Wanyamapori, maeneo ya kihistoria yenye Utalii wa kiutamaduni, eneo la uwekezaji mahiri (Special Wildlife Investment Concession Areas - SWICA), Uwindaji wa Kitalii na Ufugaji wa Wanyamapori
"TAWA imetenga maeneo kadhaa Kwa ajili ya kufanyika shughuli za utalii wa picha kutokana na ikolojia na aina ya vivutio vilivyopo katika maeneo hayo ikiwemo Pori la Akiba Mpanga/Kipengere eneo ambalo lina maporomoko ya maji zaidi ya 10 ambayo hutoa burudani safi kwa watalii" amesema Daud Tesha
Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi Wote kutembelea banda la TAWA Ili kupata maelezo ya fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika taasisi hiyo.
"Kama kauli mbiu ya Maonesho haya inavyosema kuwa Tanzania ni Mahali Sahihi pa Biashara na Uwekezaji, nitumie fursa hii kuwaambia watanzania wote kuwa TAWA ni Taasisi sahihi kwa biashara na uwekezaji kwani inatoa fursa za uwekezaji wa aina mbalimbali kama vile ujenzi wa loji, kumbi za mikutano katika maeneo yetu, kambi za watalii, michezo ya watoto lakini kama haitoshi mwekezaji anaweza akatumia fursa ya kuwekeza katika mashamba ya wanyamapori, bustani za wanyamapori n k" amesema Maganja
"Kwahiyo hii ni fursa adhimu Kwa wawekezaji wote kutembelea banda letu ili waweze kupata ufafanuzi wa fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika taasisi yetu" ameongeza
Maonesho haya yenye Kauli Mbiu "Tanzania ni Mahali Salama Pa Biashara na Uwekezaji" yameanza 28 Juni, 2024 na yanatarajiwa kufikia tamati 14 Julai, 2024
Comments
Post a Comment