SERIKALI KUJA NA MKAKATI WA MAWASILIANO WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA- KAMISHNA LUOGA

Imeelezwa kuwa Tanzania ipo katika hatua ya maandalizi ya Mkakati wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia wenye lengo la kutoa elimu na kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya kupikia nchini. 

Hayo yametanabaishwa na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga wakati akichangia mada katika Mjadala Jukwaa la Majadiliano kuhusu Masuala ya Nishati kwa Bara la Afrika uliondaliwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), uliofanyika tarehe 16 na 17 Oktoba, 2024.

Kongamano hilo lilihusisha Serikali, Washirika wa Maendeleo, Asasi za Kiraia na Sekta Binafsi ambpo Mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe.Dkt. Doto Biteko.

Luoga amesema mkakati huo utawezesha utoaji wa  elimu ya nishati hiyo kwa makundi yote ya wananchi nchini.

Ameongeza kuwa mkakati huo ndiyo utakuwa nyenzo na silaha muhimu ya kuweza kufikia azma ya Serikali ya kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya watanzania watakuwa wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.

“ Tulipoanza safari ya matumizi ya nishati safi ya Kupikia Mwaka 2022 tulikuwa na asilimia isiyozidi 10 ya kaya zinazotumia nishati safi lakini kiasi hiki kitakuwa kimeongezeka sana kutokana na juhudi zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi katika kuhamasisha matumizi ya teknolojia za nishati safi." Amesema Kamishna Luoga 

Mwezi Mei, 2024 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa Ajenda ya Matumizi ya Nishati ya Kupikia alizindua Mkakati wa Miaka 10 wa Kitaifa wa Nishati safi ya Kupikia ambao umeelekeza kuwa asilimia 80 ya watanzania wote wawe wamehamia katika matumizi ya Nishati safi ya Kupikia ifikapo mwaka 2034.

Viongozi wengine walioshiriki Kongamano hilo ni  Mha.Felchesmi Mramba,  Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati,  Dkt Kevin Kariuki, Makamu wa Rais wa AfDB na Wakuu wa Taasisi za TANESCO, REA, TPDC na EWURA.

Comments