TANZANIA YAINADI SEKTA YA NISHATI KIMATAIFA

Ili kuendelea kuifungua nchi Kimataifa, Tanzania inaendelea kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji katika Sekta ya Nishati kimataifa ikiwemo mpango wa kunadi vitalu vilivyo wazi nchini kwa ajili ya utafutaji wa mafuta na Gesi Asilia.

Hayo yameelezwa leo Novemba 5, 2024 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio kwenye Kongamano la Wiki ya Nishati 2024 (Africa Energy Week - AEW) ambalo linawakutanisha wadau wa nishati ya mafuta, gesi asilia na nishati jadidifu kutoka barani Afrika na nchi nyingine duaniani jijini Cape Town, Afrika Kusini. 

"Tanzania inatumia kongamano hili kueleza fursa nyingine za uwekezaji katika vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia alivyopewa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na fursa zilizopo katika mkondo wa kati na wa chini wa petroli ikiwemo miradi ya Mini LNG." Amesena Dkt. Mataragio

Ameongeza kuwa, Mamlaka ya Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) itakuwa na banda la maonesho kwa kushirikiana na TGS ambapo masuala mbalimbali ya mkondo wa juu wa petroli yataoneshwa pamoja na maandalizi ya duru ya tano ya kunadi vitalu vya utafutaji mafuta na gesi asilia vilivyo wazi nchini. 

Katika hatua nyingine, Dkt. Mataragio ameeleza kuwa, kongamano la AEW litavutia washiriki wengi duniani kwakuwa limekidhi mwelekeo wa dunia wa kuondokana na nishati chafuzi za mazingira.

Ameongeza kuwa, washiriki kutoka Tanzania wataweza kukutana na kampuni mbalimbali za mafuta na gesi asilia duniani ikiwemo Schlumber Company Ltd. 

Kwa mwaka 2024, kongamano hilo ni la 30 na linafanyika kuanzia tarehe 4 hadi 8 novemba nchini humo na kuhusisha wadau wa nishati zote duniani.




Comments